Wadau wa elimu waitaka serikali hamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu, Korr
Na JB Nateleng
Wadau wa elimu katika eneo la Manyatta Lengima lililoko wadi ya Korr, eneo bunge la Laisamis ,wametoa wito kwa serikali kupitia Idara ya elimu jimboni Marsabit, kuhakikisha watoto katika eneo hilo wanapata haki yao ya elimu.
Hii ni kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi inayoshudiwa katika shule ya msingi ya St. Dominic Savior.
Kwa mujibu wa Naibu Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Moses Leado, idadi hiyo imechangiwa na ukosefu wa hamasa ya kutosha kwa wazazi kuhusu umuhimu wa elimu.
Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapeleka watoto shule na baadaye kuwatoa ili kwenda kuchunga mifugo, hali inayochangia kupungua kwa idadi ya wanafunzi shuleni.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mzee wa kijiji cha Manyatta Lengima na mweka hazina wa shule hiyo, Anthony Mbalanga, ambaye amesema watoto wengi hukosa kurejea shuleni baada ya likizo kwa sababu hupelekwa maeneo ya mbali kulisha mifugo.
Naye Mkurugenzi wa Elimu katika jimbo katoliki la Marsabit, Padri Abraham Ali, ameitaka serikali kuangazia changamoto zinazowakumba wakaazi wa eneo hilo na kuanzisha kampeni za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu.
Kando na changamoto ya elimu, wakaazi hao pia wamelalamikia ukosefu wa huduma za afya wakisema hulazimika kusafiri umbali mrefu kutoka Manyatta Lengima hadi Namarei kutafuta matibabu.
Wamesema wanawake wajawazito ndio wanaoathirika zaidi kutokana na safari ndefu za kutafuta huduma za afya, hali ambayo wakati mwingine husababisha vifo.
Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa viongozi waliochaguliwa kuzuru maeneo ya mashinani mara kwa mara na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi badala ya kukaa mijini pekee.



Post Comment