Viongozi wa dini ya Kiislamu waungana kupinga ukeketaji, Marsabit Central
Na JB Nateleng
Viongozi wa dini ya Kiislamu katika kaunti ndogo ya Marsabit Central eneo bunge la Saku kaunti ya Marsabit wamepokezwa mafunzo kuhusu madhara ya ukeketaji pamoja na njia mbadala za kupambana na mila hiyo iliyopitwa na wakati.
Wakizungumza baada ya kukamilisha mafunzo ya siku tatu yaliyolenga masuala ya dini na ukeketaji, viongozi hao 30 wa dini wamesema kuwa ukeketaji ni dhuluma dhidi ya watoto wa kike wakiahidi kuendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara yake.
Wamesisitiza kuwa dini ya Kiislamu hairuhusu mtoto wa kike kukeketwa, huku wakihimiza jamii kuachana na mila hiyo ambayo inaathiri afya elimu na maisha ya mtoto msichana.
Hata hivo mwenyekiti wa Baraza la Maimam na Wahubiri nchini (CIPK) kaunti ya Tana River, Ustadh Abdillahi Haji, ambaye alikuwa mkufunzi katika warsha hiyo, amesema viongozi wa kidini wana jukumu muhimu la kuielimisha jamii kuhusu mila zilizopitwa na wakati na kuwahamasisha wananchi kukumbatia mabadiliko chanya yatakayochangia maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la MWADO, Nuria Gollo, amesema jamii inapaswa kuelewa kuwa hakuna dini inayoruhusu ukeketaji akiongeza kuwa mila hiyo inafaa kukomeshwa kabisa kwa manufaa ya watoto wa kike.
Katika hafla hiyo, Masheikh sita waliteuliwa kusaidia kutafsiri na kuelezea sheria zinazolinda mtoto wa kike, hasa kuhusu ukeketaji, ili kuelimisha jamii ya Kiislamu kuhusu umuhimu wa kupinga mila hiyo.
Aidha, juhudi hizo zitasaidia kuandaliwa kwa kitabu kitakachotumiwa na masheikh pamoja na viongozi wa dini ya Kiislamu katika kaunti ya Marsabit kuhamasisha jamii dhidi ya ukeketaji.
Hatua hiyo inaaminika kusaidia zaidi katika vita vya kukomesha mila hiyo potovu.



Post Comment