Shule 27 Marsabit zakumbatia teknolojia dijitali.
Na JB Nateleng
Shule 27 katika kaunti ya Marsabit zimeanza kutumia teknolojia ya kidijitali katika masuala ya elimu, hatua inayotarajiwa kuboresha kiwango cha elimu jimboni.
Haya yamethibitishwa na Afisa wa Elimu Marsabit, Gollo Guyo, ambaye amesema kupitia ushirikiano kati ya idara ya elimu na wadau mbalimbali, idadi ya shule zinazotumia teknolojia imeweza kuongezeka kutoka 12 hadi 27 kwa sasa.
Gollo amesema idara ya elimu itaendelea kuwekeza zaidi katika matumizi ya teknolojia katika shule zote za hapa mjini na hata mashinani.
Kauli yake imeungwa mkono na Abdullahi Hassan kutoka Baraza la Maendeleo la Kaunti za Mipakani (FCDC), ambaye amesema kuwa wataendelea kushirikiana na idara ya elimu kubuni njia bora za kuwafunza wanafunzi jinsi ya kutumia teknolojia kwa njia sahihi na iliyo bora.
Kwa upande wake, Mwalimu David Adonai, ambaye alitangazwa mshindi wa wiki iliyopita wa mashindano ya Uvumbuzi Entrepreneurship Challenge, amesema walimu pamoja na wanafunzi wanaendelea kuvutiwa na matumizi ya teknolojia mashuleni.
Amesema teknolojia inasaidia walimu kupanga kazi zao pamoja na kuwasaidia wanafunzi kufanya mazoezi ya ziada darasani.
Hata hivyo, Adonai ametaja uhaba wa vifaa vya teknolojia pamoja na upungufu wa walimu wenye ujuzi wa kidijitali kuwa changamoto zinazokwamisha matumizi ya teknolojia katika baadhi ya shule za Marsabit.
Walimu na wanafunzi wamempongeza Mwalimu Adonai kwa ushindi wake katika mashindano hayo ya Uvumbuzi, wakisema hatua hiyo itawapa motisha walimu wengi zaidi kukumbatia matumizi ya teknolojia katika elimu.



Post Comment