Highlights

Ngamia 4 wauawa katika shambulizi la wizi wa mifugo, Kambinye

Na Caroline Waforo

Ngamia wanne wameuawa, sita wakijeruhiwa huku wengine 3 wakiibwa katika shambulizi la wizi wa mifugo lililotokea alfajiri ya leo Alhamisi katika eneo la Kambinye kaunti ya Marsabit.

Akithibitisha kisa hicho, kaimu kamanda wa polisi kaunti ya Marsabit George Kipkoros amesema shambulizi hilo lilitekelezwa katika eneo la malishoni. 

Kipkoros amethibitisha kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulizi hilo.

Amesema operesheni kali ya kikosi cha kupambana na wizi wa mifugo (ASTU) kwa ushirikiano na maafisa wa RDU, DCI pamoja na maafisa wa akiba NPR imefanikisha kurejeshwa kwa ngamia walioibwa huku vikosi hivyo vikiendelea kuwasaka washukiwa.

Vilevile ametoa onyo kali kwa wahalifu wa wizi wa mifugo akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukulia dhidi yao.

Kisa hicho kimekosolewa na mwakilishi wadi wa Karare, Joseph Leruk ambaye amevitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili wahusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Aidha, ameitaka jamii kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahalifu wanaovuruga amani katika eneo hilo.

Leruk pia amesema kuwa kupitia ushirikiano kati ya viongozi, jamii na wadau mbalimbali, kuna haja ya kuendelea kuhimiza amani na kuishi pamoja kwa mshikamano.

Post Comment