Nauli za mabasi Moyale–Nairobi zapanda huku abiria wakilalamika
Na Samuel Kosgei
Wawakilishi wa wafanyabiashara pamoja na washikadau wa sekta ya usafiri wa umma mjini Moyale wamelalamikia vikali hatua ya wamiliki wa mabasi yanayosafiri kati ya Moyale na Nairobi kuongeza nauli, wakisema hatua hiyo itaendelea kuwaumiza abiria.
Ahmed Ali ambaye ni mwakilishi wa wafanyabiashara na msimamizi wa watumiaji wa magari ya umma mjini Moyale, amesema kupitia Radio Jangwani kuwa abiria walipaswa kuhusishwa katika maamuzi hayo kabla ya kutekelezwa, akieleza kuwa wakazi wengi wa eneo hilo kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Ali sasa anazitaka kampuni za mabasi kutafakari upya uamuzi huo, akidai kuwa umefanywa kwa haraka bila kuzingatia uwezo wa kifedha wa abiria wengi.
Hata hivyo, wamiliki wa kampuni 10 za mabasi katika kaunti ya Marsabit wamesema hatua yao imesababishwa na kupanda kwa bei ya dizeli hali ambayo imeongeza gharama za uendeshaji.
Kufuatia ongezeko hilo jipya, nauli ya safari ya Moyale hadi Nairobi sasa itakuwa shilingi elfu 3,500, Marsabit hadi Nairobi shilingi elfu 3,000 huku Nairobi hadi Isiolo ikiwa shilingi elfu 1,500.



Post Comment