Mwanaharakati awataka viongozi wanawake kutetea haki za kina mama.
Na Nyabande Orwa
Afisa mkuu wa shirika la Marsabit Women Advocacy and Development (MWADO) Nuria Golo ametoa wito kwa wanawake walioko katika nafasi za uongozi katika sekta mbalimbali kutetea maslahi ya kina mama wenzao. Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa katika jamii.
Akizungumza na kituo hiki mapema leo katika kipindi cha Amkia Jangwani, Nuria amesema changamoto nyingi zinazowakumba wanawake katika uongozi zinaweza kutatuliwa pale wanawake walioko madarakani watakapotumia nafasi zao kuwainua na kuwatetea wanawake wengine.
Aidha, amewakosoa baadhi ya viongozi wanawake wanaoshindwa kutetea maslahi ya kina mama. Hata hivyo amesema kuwa wakati mwingine matokeo ya juhudi hizo huenda yasionekane mara moja, hasa wakati ambapo kila mtu anapigania nafasi yake katika jamii.
Wakati huo huo, Nuria amesema licha ya serikali kuu na zile za kaunti kuweka sera na sheria za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi, changamoto kubwa bado ni utekelezaji wa sheria hizo.
Amewahimiza wananchi pia kuunga mkono juhudi za kuinua mtoto wa kike kwa kuwachagua viongozi kwa kuzingatia uwezo wao wa kuongoza, badala ya kuangalia jinsia au kabila lao.



Post Comment