Mwanafunzi wa miaka 14 afariki wakati wa maandamano mjini Moyale
Na Caroline Waforo
Mwanafunzi wa miaka 14 amefariki dunia baada ya kupigwa risasi tumboni, huku watu wengine wanne wakijeruhiwa wakati wa maandamano mjini Moyale leo Alhamisi.
Naibu kamisha wa Moyale Benedict Munywoki amethibitisha tukio hilo akisema kuwa mvulana huyo alifariki dunia akipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Moyale huku majeruhi wakiendelea kupokea huduma.
Maandamano hayo ya kupinga kile waandamanaji wanasema ni unyakuzi wa ardhi ya Basir yaligeuka na kuwa makabiliano kati yao na maafisa wa polisi.
Katika vurugu hizo jenereta ya benki ya Equity iliteketezwa huku gari moja la polisi likiharibiwa vibaya.
Vile vile biashara zilisalia kufungwa mchana kutwa huku uchukuzi ukitatizika katika barabara ya Moyale-Marsabit.
Katika mji wa Marsabit maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kutawanya waandamanaji.
Akizungumza katika kikao cha kuwasilisha mapendekezo ya miradi ya maendeleo ya maeneo bunge kwa mwaka wa kifedha wa 2026/2027 katika ukumbi wa kanisa Katoliki, Naibu Kamishna wa Marsabit Stephen Kiloi amewataka wakaazi kudumisha amani wakati wa maandamano huku akitoa hakikisho kuwa suluhu ya kudumu kwa mzozo wa Basir itapatikana kwa haraka.



Post Comment