Highlights

Marsabit yashuhudia idadi ndogo ya wanafunzi wanaojiunga na Gredi ya 10 siku ya kwanza.

NA Nyabande Orwa

Wanafunzi wa gredi ya kumi wameanza kujiunga na shule mbalimbali walizopangiwa katika kaunti ya Marsabit. Hata hivyo, idadi ya wanafunzi waliojitokeza siku ya kwanza imekuwa ndogo.

Katika baadhi ya shule mjini Marsabit tulizotembelea, wanafunzi waliofika walikuwa wachache ikilinganishwa na idadi ya nafasi zilizotolewa na wizara ya elimu.

Katika shule ya upili ya mseto ya Marsabit, idadi ya wanafunzi waliojitokeza ilikuwa ya wastani. Zoezi la kujiandikisha lilianza mapema, huku wazazi wakiandamana na watoto wao shuleni.

Wakati huo huo, katika shule ya upili ya wasichana ya Moi, idadi ya wanafunzi waliojitokeza kujiandikisha ilikuwa ndogo sana. Hata hivyo, uongozi wa shule unasema huenda idadi ikaongezeka kadri siku zinavyosonga kabla ya Ijumaa wiki hii.

Kule Moyale, katika shule ya upili ya St Mary, wanafunzi wapatao sabini pekee ndio waliokuwa wamejiandikisha kufikia mapema leo, huku zoezi hilo likiendelea.

Baadhi ya walimu wakuu wanasema idadi ndogo ya wanafunzi imesababishwa na wanafunzi kubadilisha shule walizopangiwa.

Kwa upande wao, wazazi wanalalamikia watoto wao kupangiwa shule za mbali. Wanasema hawana uwezo wa kuwapeleka watoto hao mbali na nyumbani kutokana na gharama kubwa ya karo na usafiri.

Wazazi waliozungumza na kituo hiki wameipongeza wizara ya elimu kwa kuruhusu wanafunzi kubadilisha shule, wakisema hatua hiyo itawasaidia kutokana na changamoto za kifedha.

Huku hayo yakijiri

Biashara za kuuza sare za shule katika kaunti ya Marsabit zimeandikisha idadi ndogo ya wanunuzi wiki hii, huku wanafunzi wa gredi ya kumi wakijiunga na shule mbalimbali katika kaunti hii.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na meza yetu ya habari wamesema hali hiyo imesababishwa na shule nyingi kuamua kushona sare zao wenyewe, badala ya kuzinunua katika maduka ya mjini.

Wafanyabiashara hao wanasema biashara ya sare ilinoga tu wakati wa kufunguliwa kwa shule, hasa kwa wanafunzi wa madarasa ya chini waliokuwa wakirejea shuleni.

Hali ni kama hiyo kwa wauzaji wa mabegi ya shule. Wanasema wazazi wengi wanalalamikia hali ngumu ya uchumi, hali inayowalazimu kuangazia kwanza mahitaji ya kimsingi, huku masuala ya elimu yakipewa kipaumbele cha mwisho.

Post Comment