Wananchi Marsabit watahadharishwa dhidi ya kujihusisha na visa vya kulipiza kisasi
Na Caroline Waforo
Kamati ya usalama katika kaunti ya Marsabit imetahadharisha jamii dhidi ya kujihusisha na visa vya kulipiza kisasi kufuatia shambulizi la hivi punde la wizi wa mifugo, lililosababisha vifo vya watu wanne katika eneo la Manyatta Ginda kaunti ndogo ya Marsabit Central.
Akizungumza na wanahabari leo Jumatano wakati wa mkutano wa kamati ya usalama pamoja na ile ya amani, Kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau amethibitisha kuwa idara za usalama tayari zina majina ya washukiwa wa tukio hilo na juhudi za kuwasaka zinaendelea ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Aidha, machifu wametakiwa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha wahalifu hao wamekamatwa haraka iwezekanavyo.
Na huku visa vya utovu vya usalama vikizidi kushuhudiwa, Kamishna Kamau amesema kuwa kamati ya usalama pamoja na ile ya amani itaandaa mikutano na jamii mbalimbali ili kuimarisha mshikamano na kuzuia migogoro.
Ameongeza kuwa mkutano mwingine utafanyika hivi karibuni ukiwaleta pamoja viongozi wa kisiasa hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya amani Marsabit Sora Guyo, ameitaka jamii kuwa na subira huku uchunguzi ukiendelea, akiwahimiza wananchi kudumisha amani na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa muhimu.
Vilevile wananchi wameonywa dhidi ya kueneza propaganda mitandaoni hatua inayoweza kuchochea taharuki na kuvuruga amani.



Post Comment