Highlights

Mahakama yaungwa mkono kwa uamuzi wa mahusiano ya matineja kwa maelewano

Maamuzi ya Mahakama Kuu kwamba si kosa kwa matineja kufanya mapenzi mradi kuwe na maelewano kati yao yanaendelea kupokelewa kwa mitazamo tofauti kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu pamoja na mawakili.

Chama cha Wanasheria nchini LSK tawi la Marsabit, kikiongozwa na mwakilishi wake wakili John Behailu, kimesema kuwa maamuzi hayo yanakaribishwa kwani kwa muda mrefu mvulana ndiye amekuwa akibebeshwa lawama pekee huku msichana akionekana kama mwathiriwa.

Anasema uamuzi huo sasa unafungua nafasi kwa mtoto mvulana pia kusikilizwa, mradi tu kitendo hicho kilifanyika kwa maelewano kati ya pande zote mbili.

Hata hivyo, ameonya kuwa bado ni kinyume cha sheria kufanya kitendo hicho kwa lazima, kwa vitisho au kwa kutumia hila. Amesema adhabu bado ipo kwa wale wanaotumia nguvu au vitisho kumdhuru mtoto mwingine kimapenzi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa watetezi wa haki za binadamu hapa Marsabit, Mohammed Hassan, amepongeza maamuzi hayo akisema kuwa kwa miaka mingi mtoto mvulana amekuwa akibebeshwa mzigo wote watoto wanaposhiriki ngono kwa kuelewana.

Hata hivyo, amesema nafasi hiyo haifai kutumiwa vibaya kwani sheria bado inachukua hatua dhidi ya wale wanaotumia nguvu, vitisho au ushawishi mbaya.

Post Comment