Loading Now

Highlights

Usalama waimarishwa Isiolo, mifugo iliyoibiwa yarejeshwa kulingana na kamishna David Kiprop.

NA Nyabande Orwa

Kamishna wa kaunti ya Isiolo, David Kiprop, amesema kuwa asasi za usalama zinaendelea kuchukua hatua kuhakikisha hali ya usalama inarejea kama ilivyokuwa awali katika kaunti hiyo.

Akizungumza na kituo hiki kwa njia ya simu, Kiprop amesema maafisa wa usalama wametumwa katika maeneo yanayokumbwa na visa vya utovu wa usalama.

Amesema maafisa hao wamefanikiwa kurejesha mifugo zaidi ya 450 iliyoibiwa wiki mbili zilizopita, pamoja na mifugo 175 kati ya mifugo takriban 300 iliyoibiwa katika eneo la Garbatulla.

Kiprop ameongeza kuwa oparesheni kali inaendelea kuwasaka na kuwakamata wahuni wanaomiliki silaha kinyume cha sheria ili wawajibishwe kisheria.

Aidha, amesema usalama wa wanafunzi umeimarishwa, huku maafisa wakifanya doria za mara kwa mara ili kuhakikisha masomo yanaendelea bila kuvurugwa.

Kuhusu kisa cha kuuawa kwa mtoto wa miaka 16, Kamishna huyo amesema maafisa wa upelelezi wanaendelea na uchunguzi na wako mbioni kumkamata mshukiwa na kumfikisha mahakamani.

Cue in: CC Isiolo

Haya yanajiri saa chache baada ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Isiolo, Mhashamu Peter Munguti Makau, kutoa wito kwa washikadau na viongozi mbalimbali kuingilia kati hali ya utovu wa usalama katika kaunti ya Isiolo.

Askofu Makau amesema kuwa visa vya wizi wa mifugo vimeongezeka na kuathiri shughuli za kawaida za wakazi wa kaunti hiyo.

Ametoa wito kwa waumini wa Kanisa Katoliki, viongozi wa kidini na serikali kushirikiana ili kurejesha amani na usalama katika kaunti hiyo.

Post Comment