Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji waadhimishwa Loglogo
NA Silvio Nangori
Jamii ya loglogo katika kaunti ya marsabit leo imeungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji, siku inayolenga kuangazia madhara ya mila hiyo na kuhamasisha ulinzi wa haki za wasichana na wanawake.
Maadhimisho hayo yamelenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za kiafya, kisaikolojia na kijamii zinazotokana na ukeketaji, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vinavyokiuka haki zao.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, mmoja wa kundi la akina mama eneo la Loglogo Monica Basele, amesema juhudi za uhamasishaji zimeanza kuzaa matunda, kwani baadhi ya wanajamii wameachana na mila hiyo baada ya kuelimishwa kuhusu madhara yake. hata hivyo, amesema bado kuna changamoto kwani visa vya ukeketaji vinaendelea kufanyika kwa siri.
Basele ameongeza kuwa kupitia juhudi za vikundi vya akina mama katika eneo hilo, wamefanikiwa kujenga chumba maalum cha kuwahifadhi waathirika wa dhulma za kijinsia, ikiwemo ukeketaji na ndoa za mapema.
Amehimiza mshikamano wa jamii nzima katika kukomesha vitendo hivyo.
kwa upande wake, Afisa wa programu katika shirika la Caritas Marsabit, Rufo Barako, amesema ukeketaji ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea kuathiri maisha ya wasichana na wanawake wengi, hususan katika jamii za wafugaji.
Amesema kaunti ya Marsabit bado inaandikisha viwango vya juu vya ukeketaji kutokana na kuendelea kwa mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.
Takwimu zinaonyesha kuwa takriban wanawake na wasichana milioni 230 duniani ni waathirika wa Ukeketaji, huku karibu wasichana milioni nne wakiendelea kukumbwa na hatari ya kufanyiwa ukeketaji kila mwaka, hali inayoashiria kuwa juhudi zaidi zinahitajika kukomesha mila hiyo.
Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji eneo la loglogo yameandaliwa na shirika la caritas marsabit, kwa ushirikiano na mashirika mengine ya kijamii kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa wasichana na kuhimiza jamii kuachana kabisa na ukeketaji.



Post Comment