Loading Now

Highlights

Pendekezo la chemical castration lazua mjadala mkali Marsabit

NA Nyabande Orwa

Siku chache baada ya ripoti ya jopo kazi la kuangazia ukatili wa kijinsia (GBV) pamoja na mauaji ya wanawake na wasichana (femicide) kupendekeza kuwa wanaume wanaopatikana na hatia ya makosa hayo wawajibishwe kupitia ulemazaji wa homoni za uzazi kwa dawa, almaarufu kama chemical castration, wadau mbalimbali wameendelea kutoa maoni kinzani kuhusu pendekezo hilo.

Kwa mujibu wa wakazi waliozungumza na kituo hiki, baadhi wanaamini kuwa wahalifu wa kingono wanaothibitishwa kupitia uchunguzi wa kina na ushahidi wa kutosha wanapaswa kuadhibiwa vikali ili kuzuia kurejea kwa vitendo hivyo.

Hata hivyo, wakazi wengine wana hofu kuwa iwapo pendekezo hilo litaidhinishwa, huenda likafungua mianya ya matumizi mabaya, ambapo wanawake wanaweza kulichukulia kama kitega uchumi kwa kuwasingizia wanaume kwa nia ya kunufaika kifedha.

Wakati huo huo, upande wa kisheria una mtazamo tofauti. Wakili John Behailu wa kaunti ya Marsabit anasema pendekezo hilo halifai kuzingatiwa, akieleza kuwa baadhi ya kesi za ukatili wa kingono huibuka baadaye kuwa za kusingiziwa, na mara nyingine wahusika huachiliwa huru baada ya rufaa kufanikiwa.

Behailu pia anaeleza kuwa wapo watuhumiwa ambao, hata baada ya kuhukumiwa, hubadilisha tabia na kuishi kwa amani ndani ya jamii, hivyo adhabu hiyo inaweza kuwa ya kudumu hata pale haki mtuhumiwa anapata haki.

Gumzo hili linakuja baada ya Jopo kazi lililoongozwa na Dkt. Nancy Baraza, aliyewahi kuwa naibu Jaji Mkuu, kuwasilisha rasmi ripoti yake kwa Rais William Ruto mnamo tarehe 26 Januari 2026, Ikulu ya Nairobi.
Ripoti hiyo ilipendekeza mabadiliko mbalimbali ya kisheria, ikiwemo kurekebishwa kwa sheria ya makosa ya ngono ya mwaka 2006 ili kuingiza adhabu ya chemical castrationkwa wahalifu wa ngono, hasa wale wanaopatikana na hatia ya kuwanyanyasa watoto na watu wenye ulemavu.

Post Comment