Mvua na ngurumo kutarajiwa Marsabit, upepo mkali kuathiri baadhi ya maeneo
Na Samuel Kosgei
Utabiri wa hali ya hewa wa siku saba kuanzia tarehe 24 hadi 30 Machi mwaka 2026 unaonyesha kuwa sehemu mbalimbali za kaunti ya Marsabit zinatarajiwa kushuhudia mvua za asubuhi, pamoja na manyunyu ya alasiri na usiku, zitakazoandamana na ngurumo za radi.
Maeneo yatakayopokea mvua hizo ni pamoja na Sagnante, Karare, Uran, Obbu, Butiye, Golbo, Manyatta Hellu na baadhi ya maeneo ya Maikona.
Kwa mujibu idara hiyo ya utabiri, maeneo ya kaskazini-mashariki mwa kaunti yana uwezekano wa kupokea kiwango kikubwa zaidi cha mvua ikilinganishwa na maeneo mengine.
Wakati huo huo, upepo wa wastani hadi mkali kutoka kusini na kusini-mashariki unatarajiwa kuvuma katika maeneo mengi ya kaunti.
Hata hivyo, wakazi wa eneo la Loyangalani wameonywa kujiandaa kwa upepo mkali zaidi utakaovuka mafundo 25, hali inayoweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo vumbi kali na usumbufu wa shughuli za kawaida.
Wananchi wanashauriwa kuchukua tahadhari hususan katika maeneo yatakayopokea mvua nyingi na upepo mkali.



Post Comment