Loading Now

Highlights

Hatua ya kutimuliwa kwa Edwin Sifuna kama katibu mkuu wa ODM yaendelea kuibua hisia mseto Marsabit

NA JB Nateleng

Hatua ya kamati Kuu ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kumfurusha Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kama Katibu Mkuu wa chama hicho imeendelea kuibua hisia mseto miongoni mwa wananchi.

Katika Kaunti ndogo ya Marsabit Central, baadhi ya wakazi waliozungumza na idhaa hii wamesema kwamba Sifuna amekuwa kama nguzo muhimu katika chama cha ODM na kutimuliwa kwake kama katibu mkuu huenda kukasambaratisha chama hicho.

Vilevile wamemhimiza Sifuna kuungana na upinzani ili kuendeleza ajenda ya kutetea wananchi dhidi ya serikali tawala.

Hata hivyo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amesema kwamba kutimuliwa kwake ni vita vya kisiasa kutoka kwa baadhi ya viongozi  nchini.

Akizungumza na wanahabari hii leo Sifuna amesisitiza kwamba yeye ni mwanachama wa ODM na ataendelea kuhudhuria vikao vyote vya ODM.

Aidha Jopo la kusuluhisha mizozo ya vyama vya kisiasa limesimamisha kwa muda kutimuliwa kwa Edwin Sifuna katika nafasi ya Katibu Mkuu hadi malalamiko aliyowasilisha yatakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.

Post Comment