Wazee wa Yaa Algana watoa wito wa umoja Marsabit
Na JB Nateleng
Wazee kutoka Baraza la Jamii ya Gabra, Yaa Algana, kaunti ya Marsabit wametoa wito kwa viongozi jimboni kuungana na kuweka mbele maslahi ya wananchi ili kuimarisha umoja, amani na maendeleo.
Wakizungumza na idhaa hii, wazee hao wamesema kuwa ingawa wananchi wana mitazamo na misimamo tofauti hasa wakati wa uchaguzi, jambo la msingi linapaswa kuwa kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa jamii zote za Marsabit.
Wamesema kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko, wakisisitiza umuhimu wa viongozi kuwa mfano bora kwa kuhubiri na kuendeleza umoja.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwanasiasa Umuro Roba, ambaye amewahimiza wakaazi wa Marsabit kuwachagua viongozi kwa kuzingatia manifesto zao za maendeleo badala ya kuegemea misingi ya chama au kabila.
Amedai kuwa siasa za ukabila na ufuasi wa vyama bila kuangalia ajenda za maendeleo zimechangia kwa kiasi kikubwa kudorora kwa maendeleo.
Aidha, Roba amewataka wanasiasa kuwa waangalifu wanapozungumza na wafuasi wao, akionya kuwa maneno ya uchochezi yanaweza kusababisha vurugu na kuvuruga amani ya jamii wakati wa kampeni.



Post Comment