Loading Now

Highlights

Wachukuzi katika barabara ya Loiyangalani-Marsabit walalamikia hasara kutokana na ubovu wa barabara

Na JB Nateleng

Wachukuzi wa magari katika barabara ya Loiyangalani-Marsabit wamelalamikia hasara kubwa kufuatia hali mbaya ya barabara iliyofurika maji, hali inayozorotesha shughuli za usafirishaji.

Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya kipekee, msimamizi wa magari ya uchukuzi Loiyangalani, Mzee Abdi, amesema kuwa safari zimekuwa ngumu na za muda mrefu, jambo linalochangia hasara kwa wamiliki wa magari.

Ameeleza kuwa kwa sasa magari yanachukua muda mrefu zaidi kufika Marsabit, akitoa mfano wa tukio la hivi majuzi ambapo gari moja lilichukua siku mbili kukamilisha safari hiyo.

Mzee Abdi sasa anatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kutengeneza barabara hiyo ili kurahisisha usafiri na kuokoa sekta ya uchukuzi katika eneo hilo.

Mvua iliyonyesha mwishoni mwa wiki jimboni Marsabit imesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali, ikiwemo barabara na nyumba za wakazi, na hivyo kuongeza wasiwasi katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na changamoto za usafiri.

Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha katika sehemu mbalimbali za jimboni huku wakazi wakishauriwa kuchukua tahadhari na kujiepusha na maeneo yenye hatari.

Post Comment