Viongozi katika kaunti ya Marsabit watakiwa kuwatumikia wananchi haswa msimu huu wa ukame.
NA JB Nateleng
Viongozi katika kaunti ya Marsabit wametakiwa kuweka mbele maslahi ya wananchi huku wataalamu wa hali ya hewa wakitabiri kuwa huenda kaunti ya Marsabit likapokea mvua ya kiwango cha kawaida hadi chini ya kawaida katika msimu wa Machi hadi Mei mwaka huu.
Kwa mujibu wa mwanasiasa Abdikadir Doyo, hali hiyo inazidi kuzorotesha maisha ya wakazi wengi ambao tayari wanakabiliwa na changamoto kufuatia mvua chache zilizonyesha katika msimu wa Oktoba, Novemba na Desemba mwaka uliopita.
Doyo amesema upungufu wa mvua ulioshuhudiwa mwishoni mwa mwaka uliopita umeathiri pakubwa uzalishaji wa chakula na upatikanaji wa malisho, hali iliyosababisha familia nyingi kuhitaji msaada wa chakula na mahitaji mengine muhimu.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi katika kaunti ya Marsabit kuwa makini na masuala yanayowaathiri wakazi, hasa kipindi hiki ambacho ukame unatishia ustawi wa jamii.
Aidha, Doyo amewahimiza wananchi kujiepusha na siasa za ukabila wakati wa uchaguzi, akisema kuwa ni muhimu kuchagua viongozi kwa misingi ya uadilifu na uwezo wa kushughulikia changamoto zinazoikumba kaunti ya Marsabit.
Wito huu unajiri siku moja tu baada ya kukamilika kwa kongamano la siku tatu la IGAD kuhusu utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa Machi hadi Mei katika ukanda wa kusini mwa Ethiopia na kaunti ya Marsabit. Kongamano hilo lilifanyika nchini Ethiopia na kuwaleta pamoja wataalamu kutoka idara za utabiri wa hali ya hewa, mamlaka za kushughulikia majanga pamoja na wanahabari.



Post Comment