Loading Now

Highlights

NCCK Marsabit yalaani mashambulizi ya nyumba za ibada.

NA Joseph Muchai

Uongozi wa muungano wa makanisa nchini (NCCK) katika kaunti ya Marsabit umekemea vikali mashambulizi yaliyotokea katika kanisa la ACK Watima Othaya kaunti ya Nyeri siku ya Jumapili.

Akizungumza na Shajara ya Radio Jangwani, mwenyekiti wa NCCK Marsabit, mchungaji Said Diba, amesema tukio hilo halikubaliki, hasa likihusisha vyombo vya usalama.

Diba amesema uhuru wa kuabudu umeingiliwa na kudhalilishwa, akibainisha kuwa hapo awali sehemu za ibada ziliheshimiwa na hata kutumika kama maeneo ya usalama wakati wa hatari, hali ambayo anasema sasa inaonekana kubadilika.

Ameongeza kuwa huku joto la kisiasa likizidi kupanda, wanasiasa wanapaswa kuheshimiana ili kulinda usalama na mshikamano wa taifa na kutoa wito kwa sheria kufuatwa ili kuzuia dhuluma dhidi ya raia wasio na hatia.

Kauli hiyo inajiri siku moja baada ya waumini kushambuliwa kwa gesi ya kutoa machozi na risasi za moto wakati aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, alipohudhuria ibada ya kanisa katika kaunti ya Nyeri.

Post Comment