Mwanaume mmoja ahukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kumnajisi msichana wa miaka 9, Marsabit South
Mahakama ya Marsabit imemhukumu kifungo cha maisha gerezani mwanaume mmoja kwa kosa la kumnajisi msichana mwenye umri wa miaka 9 katika lokesheni ya Namarei kaunti ndogo ya Marsabit South.
Lerasho Lekaata amepatikana na hatia ya kumnajisi msichana huyo mnamo tarehe 9 mwezi Novemba mwaka 2024.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne na aliyekuwa hakimu mwandamizi wa mahakama ya Marsabit Simon Arome aliyepewa uhamisho.
Mshtakiwa ana siku 14 kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Wakati uo huo
Mwanaume aliyetuhumiwa kumuua mwanaume mwenzake kwa kumdungwa kisu majuma kadhaa yaliyopita, kutokana na mzozo wa kimapenzi katika eneobunge la North Horr amefunguliwa mashtaka ya mauaji katika mahakama kuu ya Marsabit.
Mshukiwa Guyo Talbe anakabiliwa na tuhuma na kumuua Badaqe Galgallo Abduba kufuatia mzozo ulioibuka baada ya wawili hao kukutana katika nyumba ya mwanamke mmoja ambaye mume wake alikuwa amesafiri kikazi katika kaunti jirani ya Isiolo
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani tarehe 11 mwezi huu wa Februari ambapo mshukiwa alikana mashtaka dhidi yake mbele ya Jaji wa mahakama kuu ya Marsabit Francis Rayola.
Aidha Jaji Rayola ameipa idara ya probesheni siku 21 kuwasilisha ripoti kuhusu mshukiwa huyo huku kesi hiyo ikitarajiwa kutajwa tarehe 18 mwezi ujao wa Machi.



Post Comment