Highlights

Mvutano ndani ya ODM wazidi kupamba moto vijana Marsabit wataka pande zote kukaa meza moja

Na Nyabande Orwa

Wakati mzozo ukiendelea ndani ya chama cha ODM kati ya upande wa katibu mkuu Edwin Sifuna na upande unaomuunga mkono kiongozi wa chama Dkt. Oburu Oginga, viongozi wa vijana wa chama hicho katika kaunti ya Marsabit wametoa wito wa amani na maelewano.

Vijana hao wanasema pande zote zinapaswa kukaa pamoja na kusuluhisha tofauti zao kwa manufaa ya chama.

Kwa mujibu wa Stephen Basele, ambaye ni mjumbe wa kamati ya kitaifa ya uamuzi ya ODM (NEC), mvutano unaoendelea kwa sasa pia umeongeza mjadala na umaarufu wa chama hicho. Hata hivyo, Basele anaonya kuwa iwapo mzozo huo hautatatuliwa mapema, unaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama.

Basele pia ameshauri mazungumzo kuhusu uwezekano wa muungano kati ya ODM na UDA yafanywe kwa uwazi, na wanachama wote washirikishwe ili kuepuka malalamiko au migogoro baadaye. Amesema kwa sasa chama bado hakijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mwelekeo wa mazungumzo hayo.

Haya yanajiri siku chache baada ya baadhi ya wakazi wa Marsabit kutoa maoni tofauti kufuatia hatua ya ODM kumtimua Edwin Sifuna, kabla ya mahakama inayoshughulikia migogoro ya vyama vya kisiasa kuamuru arejeshwe.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na idhaa hii wamesema Sifuna amekuwa nguzo muhimu ndani ya ODM, na kuondolewa kwake katika nafasi ya Katibu Mkuu kunaweza kudhoofisha chama hicho.

Post Comment