Mshukiwa wa ulawiti asakwa Logo Logo.
Na Nyabande Orwa
Maafisa wa usalama wanaendelea kumsaka mshukiwa wa tukio la kulawiti lililoripotiwa katika eneo la Logo Logo, kaunti ya Marsabit.
Kwa mujibu wa chifu wa Logo Logo, Andrew Korolle, mshukiwa anayekadiriwa kuwa na umri wa takriban miaka 16 alitoroka baada ya kumlawiti mvulana wa miaka 10 walipokuwa malishoni siku ya Jumapili.
Korolle amesema kuwa wakazi waliokuwa malishoni wakichunga mifugo ndio walioshuhudia tukio hilo na kutoa taarifa kwa ofisi ya chifu.
Kwa sasa, mtoto aliyeathiriwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Laisamis.
Wakati huo huo, chifu huyo amewataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kusaidia kuzuia matukio kama hayo. Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kwenda shule wanahudhuria masomo badala ya kupelekwa malishoni.
Aidha, amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama wanaposhuhudia visa kama hivi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.



Post Comment