Maafisa wa usalama watakiwa kuheshimu haki za raia huku operesheni ya kurejesha mifugo 3908 walioibwa ikiendelea, Loiyangalani.
NA JB Nateleng
Mwakilishi wadi wa Loiyangalani Daniel Emojo, amewataka maafisa wa usalama kuheshimu na kulinda haki za wakaazi wa Sarima kufuatia oparesheni ya kiusalama inayoendelea katika eneo hilo ya kurejesha mifugo 3908, walioibwa mwishoni mwa mwaka jana na ambayo imesababisha hasara kwa wafugaji baada ya mbuzi kufariki pamoja madai ya kujeruhiwa kwa mtoto mmoja.
Akizungumza na Shajara Emojo amesema kwamba oparesheni hiyo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia haki za binadamu, akionya dhidi ya kuumizwa raia wasiokuwa na hatia.
Emojo amesisitiza kuwa oparesheni hiyo inapaswa pia kufanyika kwa usawa.
Aidha Mwakilishi wadi huyo ameitaka Mamlaka ya kusimamia utendakazi wa Polisi (IPOA) kuchunguza kisa cha mtoto wa miaka 13 aliyejeruhiwa kwa risasi katika vuta ni kuvute iliyozuka wakati wa oparesheni hiyo.
Hata hivyo Emojo amewarai wakaazi wa Loiyangalani kudumisha amani na kushirikiana na vyombo vya usalama ili kurejesha hali ya utulivu katika eneo hilo.
Na kutokana na madai hayo ya mtoto kuumizwa na maafisa wa polisi Kamanda wa polisi katika kaunti ya Marsabit leonard Kimaiyo amesema uchunguzi unaendelea kuhusu tuhuma hizo.
Akizungumza na kituo hiki, Kimaiyo amesema kuwa hadi taarifa hii ikienda hewani maafisa wa polisi walikuwa wanamalizia mikakati ya kufika hospitalini anakosemekana amelazwa mtoto huyo ili kudhibitisha madai hayo.
Wakati uo huo akidhibitisha kisa cha mbuzi kuaga dunia walipokuwa wanahamishwa kutoka Sarima kuelekea Loiyangalani, kamanda Kimaiyo amesema huenda kutokana na wingi wa mbuzi hao walikosa hewa na kupoteza maisha.
Vile vile amesema kuwa oparesheni hiyo bado inaendelea hadi mbuzi wote na kondoo takriban 3908 wanaosemekana kuibiwa mwishoni mwa mwaka jana katika eneo la Rarashe, Kiwanja na Naagan watakaporejeshwa.



Post Comment