Dunia yaadhimisha siku ya jamii za wachache katika Ikulu jijini Nairobi.
NA NYABANDE ORWA
Huku dunia ikiadhimisha siku ya jamii za wachache, hapa nchini Kenya jamii hizo zimekutana Ikulu jijini Nairobi.
Wakizungumza katika kikao na Rais William Ruto, viongozi wa jamii za wachache kutoka maeneo mbalimbali wametoa wito wa kuhusishwa katika hazina ya uwezeshaji ili waweze kunufaika na kuinua maisha yao kiuchumi.
Akizungumza katika kikao hicho, msomi na mtetezi wa masuala ya elimu, Dkt. Christopher Galgalo, ambaye pia ni mtetezi wa haki za jamii ndogo ya Wayu wanaoishi kaunti ya Marsabit, amesema ni wakati mwafaka kwa serikali kuhakikisha fedha za hazina hiyo zinafikia jamii za wachache ili ziweze kujitegemea kiuchumi.
Aidha, Dkt. Galgalo ameitaka serikali kuhusisha jamii za wachache katika nafasi za uongozi, akisema wengi wao wamesoma na wana uzoefu mkubwa unaoweza kusaidia katika kutoa mwelekeo wa maendeleo nchini.
Ameeleza kusikitishwa na hatua ya jamii hizo kutengwa katika nafasi za uteuzi, hasa baada ya chaguzi.
Wakati huo huo, Jane Merwas kutoka kaunti ya Samburu amemtaka Rais William Ruto kuhakikisha utekelezaji wa usajili wa ardhi ya jamii kwa manufaa ya jamii za wachache nchini.
Kuhusu zoezi la sensa, Jane pia ametoa wito kwa rais kuweka mikakati ya kubadilisha muda wa zoezi hilo kutoka mwezi wa Agosti, akisema wengi wa jamii za wafugaji hawapatikani kipindi hicho kutokana na kuhama-hama wakitafuta malisho ya mifugo.
Akijibu malalamishi hayo, Rais William Ruto amesema serikali haitazitenga jamii za wachache, na imejitolea kutenga takribani shilingi milioni mia mbili katika bajeti yake kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu, shule, hospitali na maendeleo mengine katika maeneo yanayokaliwa na jamii hizo.



Post Comment