Loading Now

Highlights

Serikali yaachilia zaidi ya shilingi 800m ya Inua Jamii inayolenga watoto mayatima.

NA Samuel Kosgei

Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni mia nane sabini na saba kwa ajili ya kusaidia familia zinazowahudumia watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi chini ya mpango wa watoto mayatima.

Katika taarifa iliyotolewa jana Alhamisi, Wizara ya Jinsia, Utamaduni na Huduma za Watoto imesema fedha hizo zitanufaisha familia laki nne elfu thelathini na nane, mia nane na nne kote nchini chini ya mpango wa Inua Jamii.

Kila kaya itapokea shilingi elfu mbili, ikiwa ni malipo ya mwezi Novemba 2025. Malipo hayo yanatarajiwa kuanza leo ijumaa, kupitia watoa huduma wa malipo waliokubaliwa na serikali.

Wizara hiyo imesema mpango huo wa kutoa pesa kwa mayatima unalenga kuhimiza malezi na ulinzi wa watoto yatima na walio katika mazingira magumu ndani ya familia na jamii zao.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Idara ya Huduma za Watoto, Bi Carren Ageng’o mpango huo unakusudia kuboresha uandikishaji na mpito wa watoto shuleni, kuimarisha afya na lishe, kuongeza usalama wa chakula katika jamii, na kuimarisha ulinzi wa watoto.

Post Comment