Serikali kuu yaanza kufuatilia mienendo ya wanasiasa Marsabit msimu wa siasa ukianza.
NA NYABANDE ORWA
Kamishna wa Kaunti ya Marsabit, James Kamau, amesema kuwa serikali inafuatilia kwa karibu mienendo ya wanasiasa wa kaunti hii, hasa wakati huu ambapo msimu wa siasa umeanza kushika kasi.
Akizungumza na kituo hiki afisini mwake, Kamau amewataka wanasiasa kujiepusha na matamshi ya kugawanya jamii au kusababisha taharuki miongoni mwa wakazi wa kaunti ya Marsabit. Amesema viongozi wa kisiasa wana wajibu wa kuhubiri amani na umoja.
Wakati huohuo, Kamishna Kamau amewataka machifu kufuatilia kwa makini kila kijiji ili kuhakikisha watoto wote waliotimiza umri wa kwenda shule wanarudi masomoni, ikizingatiwa kuwa shule zimefunguliwa kwa muhula wa kwanza. Ameonya kuwa wazazi watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Kuhusu suala la njaa na kiangazi, Kamau amesema serikali kuu inaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayekumbwa na ukosefu wa chakula. Ameongeza kuwa mikakati inaendelea kuwekwa ili wale walioathirika zaidi wapate chakula cha msaada kwa wakati.



Post Comment