Kituo cha kompyuta chenye tarakilishi 50 chakabidhiwa Merile na Karare kuimarisha masomo ya kidijitali.
NA Samuel Kosgei
Shirika la Thika Alumni Trust, kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Kenya Drylands Education Fund (KDEF), limekabidhi rasmi kituo cha teknolojia chenye kompyuta 50 kwa Shule ya Sekondari ya Merile Mixed Senior na Shule ya Upili ya Karare, kama njia ya kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa matumizi ya kompyuta na teknolojia ya kisasa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa KDEF Ahmed Kura amesema kuwa kituo hicho cha masomo ya mtandaoni kitawapa wanafunzi ujuzi muhimu wa kidijitali na kuwaandaa kukabiliana na dunia ya sasa inayotegemea teknolojia.
Kura ameongeza kuwa ujio wa kompyuta hizo utawasaidia wanafunzi, hasa katika utekelezaji wa mtaala mpya wa Umilisi (CBE), ambao kwa sasa unatekelezwa kote nchini.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Merile, Francesca Delea, amelishukuru shirika la KDEF akisema kuwa uwepo wa darasa la kompyuta utachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya masomo ya STEM ambayo yanahitaji matumizi ya teknolojia.
Ameongeza kuwa shule hiyo inapanga kusajili wanafunzi wa somo la Computer Science kuanzia mwaka ujao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Upili ya Merile, mwanaharakati Rose Orguba, amesema mradi huo ni afueni kubwa kwa wanafunzi na utawasaidia kutimiza ndoto zao katika dunia ya sasa ya utandawazi.
Kura aliongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kupanuliwa na kufikia shule nyingine zikiwemo Korr Mixed, Ngurunit na Loiyangalani.



Post Comment