Kiangazi chapunguza idadi ya wanafunzi wanaoripoti shuleni kwa muhula wa kwanza, Marsabit
NA Caroline Waforo
Idadi ndogo ya wanafunzi imeripoti shuleni kwa muhula wa kwanza wa mwaka 2026 katika kaunti ya Marsabit, kutokana na makali ya kiangazi yanayoendelea kushuhudiwa.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake, Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti ya Marsabit Peter Magiri, amesema kuwa mvua chache za msimu wa Octoba hadi Disemba mwaka 2025 zimesababisha upungufu wa malisho, kukauka kwa mimea pamoja na vyanzo vya maji na hivyo kuathiri maisha ya wafugaji.
Magiri amesema shule nyingi zinatarajiwa kukumbwa na uhaba wa maji hali itakayoongeza gharama za uendeshaji wa shule, na hivyo kutoa wito kwa wadau na wafadhili mbalimbali kujitokeza na kutoa msaada.
Na huku wanafunzi wa gredi ya 10 wakitarajiwa kujiunga na shule walizoteuliwa wiki ijayo, Magiri amesema kuwa wazazi tayari wameanza kutafuta uhamisho, hasa kwa wale walioteuliwa shule za mbali, ili kumudu gharama.
Haya yanajiri huku wanafunzi 33 kutoka familia zisizojiweza wakiteuliwa kunufaika na ufadhili wa serikali wa Elimu Scholarship kupitia Jomo Kenyatta Foundation.
Kulingana na Magiri wanafunzi 9 kutoka Moyale wamenufaika na ufadhili huo, 4 kutoka Sololo, 8 Saku, 3 Laisamis, 3 Loiyangalani, 2 Chalbi, 2 Turbi huku Dukana North Horr zikipata mwanafunzi mmoja kila eneo.
Aidha wadau wengine wameombwa kuongeza juhudi zao za ufadhili wa elimu kutokana na idadi ya juu ya wanafunzi waliotuma maombi ya ufadhili huo hapa katika kaunti ya Marsabit.



Post Comment