Kanisa katoliki latahadharisha dhidi ya ongezeko la deni na ushuru lasema familia nyingi zalemewa na gharama za maisha
Na JB Nateleng
Familia nyingi nchini zinakabiliwa na maamuzi magumu kuhusu mahitaji ya kuuamua watakachopea kipaumbele kutokana na ongezeko la ushuru linaloongezeka kila uchao.
Hii ni kwa mujibu wa tathmini iliyotolewa na Kanisa Katoliki kupitia Kampeni yake ya Kwaresma ya mwaka 2026, ambayo imebainisha kuwa hadi kufikia Machi 2025, serikali ilikuwa imekopa jumla ya shilingi trilioni 11.3, sawa na asilimia 69 ya pato la taifa kiwango kinachodaiwa kuzidi kile kilichopendekezwa kikatiba.
Kupitia mafundisho ya wiki ya pili ya Kwaresma iliyo na mada ya “Ongezeko la Kasi la Deni la Serikali na Kodi ya Juu,” Kanisa limesema kuwa mzigo mkubwa umeangukia wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya kila mwezi, ambao wanakabiliwa na makato makubwa kutoka katika mapato yao.
Kwa mujibu wa Kanisa, hali hiyo imeathiri uwezo wa familia nyingi kumudu gharama za maisha, huku baadhi wakilazimika kupunguza matumizi ya mahitaji muhimu ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi.
Tathmini hiyo imesisitizwa na Padri Steve Mutuku, Baba Paroko wa Parokia ya Log Logo katika Jimbo Katoliki la Marsabit, ambaye ameikosoa serikali kwa kuendelea kuongeza ushuru bila kuangalia kwa kina hali halisi ya uchumi na uwezo wa wananchi.
Padri Mutuku amesema ushuru wa juu umewakandamiza wananchi wa kawaida na kuiomba serikali kuweka mbele ustawi wa wananchi pamoja na kufanya tathmini ya kina ya hali ya uchumi kabla ya kupitisha sera mpya za kodi.
Padri Mutuku amesema kuwa ingawa ni wajibu wa kila Mkenya kulipa kodi, ni sharti serikali ihakikishe kuwa fedha zinazokusanywa zinatumika ipasavyo ili kukidhi mahitaji ya taifa na kupunguza utegemezi wa madeni ya nje.
Baba paroko huyo amewahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa ushuru, akisisitiza kuwa kulipa kodi ni nguzo muhimu ya kujitegemea na kuijenga nchi kiuchumi.



Post Comment