Asilimia 13.5 ya Marsabit yaathirika na utapiamlo
Kaunti ndogo za Laisamis, North Horr, Moyale na Saku ndizo zilizoathirika zaidi na tatizo la utapiamlo katika kaunti ya Marsabit. Hayo yamesemwa na waziri wa afya wa kaunti ya Marsabit, Malicha Boru.
Akizungumza na kituo hiki afisini mwake, Waziri Malicha amesema Laisamis ina kiwango cha utapiamlo cha asilimia 21.5, ikifuatwa na North Horr kwa asilimia 16, Moyale asilimia 10.8 na Saku asilimia 8.7.
Malicha amesema hali hiyo imechangiwa pakubwa na ukame unaoendelea pamoja na kusitishwa kwa ufadhili kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, hususan misaada iliyokuwa ikitolewa kupitia USAID.
Ameongeza kuwa kwa ujumla, kaunti ya Marsabit ina kiwango cha utapiamlo cha asilimia 13.5, hali ambayo amesema ni ya kutia wasiwasi mkubwa.
Katika juhudi za kupunguza athari za utapiamlo, waziri Malicha amesema serikali ya kaunti imeunda timu ya pamoja ya maafisa wa afya ya umma kutoa mafunzo katika vijiji vilivyoathirika zaidi.
Amesema pia serikali ya kaunti inaendelea kushirikiana na mashirika yaliyosalia kuwafundisha wazazi namna ya kujikinga na magonjwa yanayotokana na uchafu na uhaba wa maji.
Aidha, amesema wizara hiyo inafanya kazi kwa karibu na NDMA, ili kuhakikisha chakula cha msaada kinawafikia waathiriwa wa njaa.



Post Comment