Wadau wa michezo watakiwa kushirikiana kukuza vipaji miongoni mwa vijana Marsabit
Na JB Nateleng
Vijana katika kaunti ya Marsabit wametajwa kuwa na vipaji vinavyohitaji kukuzwa kwa njia sahihi.
Haya yamebainishwa na Mratibu wa Kitengo cha Wanawake na Masuala ya Maendeleo Nchini Ronald Gideon, ambaye amesema kuwa ipo haja ya wadau wa michezo kushirikiana ili kuhakikisha vipaji miongoni mwa vijana vinatambuliwa mapema na kukuzwa ipasavyo.
Akizungumza leo baada ya uzinduzi rasmi wa michuano ya muhula wa kwanza kwa shule za sekondari katika eneo la Saku, Ronald amesema kuwa vijana 12 kutoka Marsabit tayari wamejiunga na Akademia ya Michezo ya Kenya tawi la Nyeri.
Hatua hiyo, amesema, imewavutia maafisa wa michezo kutembelea kaunti ya Marsabit ili kugundua na kukuza vipaji zaidi.
Aidha, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali ya kaunti ya Marsabit kuwekeza zaidi katika sekta ya michezo, akisema vijana jimboni wana vipaji vingi.
Kauli yake imeungwa mkono na Katibu wa michezo katika kaunti ndogo ya Saku, Hussein Sora ambaye amesema kwamba shule ambazo zimekuwa zikishiriki mashindano haya katika eneo la Saku, zimekuwa zikifuzu hadi ngazi ya kitaifa.
Mashindano haya ya kaunti ndogo ya Saku ambayo yameanza leo ijumaa yatakamilika hapo kesho Jumamosi huku shule zitakazoibuka na ushindi zikitarajiwa kumenyana na washindi sawia kutoka kaunti ndogo zote katika mashindano ya kaunti yatakayofanyika tarehe 12 hadi 13 Machi 2026 katika eneo la Saku.



Post Comment