Mvulana wa miaka 14 ashtakiwa kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa miaka 7, Marsabit Central
Na Caroline Waforo
Mvulana wa miaka 14 amekamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya Marsabit kwa tuhuma za kumlawiti mvulana mwenzake wa miaka 7 katika mtaa wa Shauri Yako kaunti ndogo ya Marsabit Central.
Akithibitisha kisa hicho cha Februari tarehe moja, OCPD wa Marsabit Central Beethoven Gachago ameeleza Shajara kuwa mshukiwa na mwathiriwa ni majirani.
Na kutokana na ongezeko la visa vya unajisi na ulawiti katika kaunti ndogo hiyo, OCPD Gachago ametoa onyo kali kwa wananchi dhidi ya kutekeleza uovu huo huku pia akitahadharisha jamii dhidi ya kusuluhisha kesi hizo mashinani.
Gachago vilevile amewataka wazazi kuwaelimisha wanao kuhusiana na makosa ya dhulma za kijinsia kwani sheria haiwasazi watoto wanaopatikana na makosa hayo.
Hapo jana Jumatano mshukiwa alikana mashtaka dhidi yake mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa mahakama ya Marsabit Christine Wekesa, na kuachiliwa kwa bondi ya shilingi 20,000 au dhamana ya pesa taslimu shilingi 5,000.
Aidha Hakimu Wekesa aliagiza idara ya watoto katika kaunti ndogo ya Marsabit Central kuwasilisha ripoti kuhusu mshukiwa huyo mahakamani.
Kesi hiyo itasikilizwa tarehe 26 mwezi huu wa Februari.



Post Comment