Loading Now

Highlights

Shule ya upili ya ACK St Andrews Marsabit, yafanya vyema kwenye mtihani wa KCSE 2025

NA JB Nateleng

Shule ya upili ya ACK St Andrews ya Badasa, eneobunge la Saku, imeandika historia baada ya wanafunzi 40 kufuzu kujiunga na vyuo vikuu kufuatia matokeo ya KCSE 2025 yaliyotangazwa wiki jana.

Wakizungumza na wanahabari baada ya kuungana na wenzao kusherehekea matokeo hayo mjini Marsabit, wanafunzi hao wakiongozwa na aliyekuwa kiranja mkuu Ali Guyo wamesema mafanikio yao yametokana na ushirikiano mzuri kati ya wanafunzi, walimu, wazazi na uongozi wa kanisa la ACK ambao waliwatia moyo mara kwa mara.

Wamewahimiza wanafunzi wenzao waliobaki shuleni kuiga mfano wao kwa kujituma zaidi masomoni ili wapate matokeo bora mwaka huu.

Kiranja mkuu wa sasa, Wako Bakaye, anasema wenzao wamewaonyesha njia ya kufuata ili kupata mafanikio zaidi masomoni.

Wakati huo huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Silvester Omondi, amesema matokeo hayo mazuri yametokana na mshikamano na ushirikiano kati ya kanisa, wazazi na walimu ambao walifanya kazi kwa bidii kuwaandaa wanafunzi kwa mtihani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa kanisa la ACK jimbo la Marsabit, Canon Kargi Denge, amesifia matokeo hayo huku akiwahimiza wanafunzi kuendelea kujituma masomoni na kuepuka udanganyifu wa mitihani akisema ni kinyume cha maadili na hakikubaliki shuleni.

Huu ulikuwa mtihani wa kwanza wa kitaifa wa KCSE kwa shule ya ACK St Andrews, ambapo imepata wastani wa alama ya B Plain, sawa na pointi 9.35.

Post Comment