Naomi Waqo asema bado yuko kwenye mbio za ugavana Marsabit 2027
Na Nyabande Orwa
Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Marsabit, Naomi Waqo Jilo, amesema hatajiondoa kwenye mbio za kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Akizungumza kwenye kipindi cha Amkia Jangwani, Naomi amesema ana uzoefu na uwezo wa kuongoza na kuendeleza kaunti ya Marsabit kama gavana.
Amesema yuko tayari kushiriki katika kura za mchujo za chama cha UDA na ataheshimu matokeo. Ameongeza kuwa iwapo hatapata tiketi, atamuunga mkono atakayechaguliwa na chama hicho.
Amesisitiza kuwa kila mgombea apewe nafasi sawa ya kujieleza kwa wananchi kabla ya maamuzi kufanywa kisiasa.
Wakati huo huo, Naomi amesema masuala ya kijinsia bado yanaathiri uchaguzi wa viongozi nchini. Amesema baadhi ya jamii hufuata maamuzi ya wazee, jambo ambalo wakati mwingine huwanyima wanawake nafasi ya uongozi.
Amewahimiza wananchi kuunga mkono uongozi wa wanawake akisema kina mama wana uwezo wa kuleta maendeleo.
Kuhusu sekta ya afya, Naomi amesikitikia hali ya huduma za afya katika kaunti ya Marsabit. Ameahidi kuwa akichaguliwa kuwa gavana, ataboresha huduma hasa kwa kina mama wajawazito na kuhakikisha kunanunuliwa magari ya kubebea wagonjwa ili kupunguza vifo vya mama na watoto.



Post Comment