Marsabit yaorodheshwa miongoni mwa kaunti 9 zilizoko kwenye tahadhari ya ukame nchini.
NA CAROLINE WAFORO
Kaunti ya Marsabit iko katika hali ya tahadhari ya ukame kutokana na kufeli kwa mvua za msimu wa mwezi October hadi Disemba mwaka huu wa 2025.
Hii ni kulingana na ripoti ya hivi punde kutoka Mamlaka ya kukabiliana na majanga NDMA tawi la Marsabit.
Hali hii pia inaendelea kuathiri ufugaji huku sasa baadhi ya wafugaji wakilazimika kutafuta malisho katika kaunti jirani.
Kule katika eneobunge la Laisamis wafugaji wamelazimika kuhama katika maeneo ya Merille, Ngurunit, Korr, Loglogo na kutafuta malisho katika maeneo ya Kom, South Horr, Kargi, Sarima na eneo la Donyo Wasin katika kaunti jirani ya Samburu.
Katika eneobunge la North Horr wafugaji wamehama maeneo ya Maikona, El Beso, Telesgaye, Dukana na kuelekea Kambi Nyoka, Idhidho, Shurr na Balesa.
Hali sawia inashuhudiwa katika baadhi ya maeneo bunge ya Saku na Moyale.
Haya ni huku ripoti ikiashiria kuwa zaidi ya watu milioni mbili nchini watahitaji msaada wa chakula katika muda wa majuma matatu yajayo, huku hofu ya ukame ikiendelea kushuhudiwa.
Idara ya utabiri wa hali ya anga imesema kuwa hali hiyo inaendelea kuongezeka katika baadhi ya kaunti huku nyingine zikianza kuingia hali mbaya.
Kaunti 9 zimeorodheshwa kuwa katika hali ya tahadhari ya ukame ikiwemo Marsabit, Mandera, Isiolo, Wajir, Garissa, Kitui, Kilifi, Tana River na kaunti ya Kajiado.



Post Comment