Marsabit miongoni mwa kaunti zinazorekodi vifo vichache vya akina mama wakati wa kujifungua
NA Caroline Waforo
Kaunti ya Marsabit imeorodheshwa miongoni mwa kaunti zilizo na idadi ndogo ya vifo vya akina mama vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Kulingana na ripoti ya Wizara ya Afya nchini ya kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka 2025, kaunti ya Marsabit imeorodheshwa katika nafasi ya 46 kati ya kaunti 47 nchini, ikimaanisha kuwa idadi ya vifo vya akina mama vilivyoripotiwa katika vituo vya afya ni vichache ikilinganishwa na kaunti nyingine nchini.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake Mkrugenzi katika idara ya Afya ya Uzazi kaunti ya Marsabit Bokayo Arero, amesema mafanikio hayo yamechochewa na kuimarishwa kwa huduma za uzazi pamoja na ushirikiano uliopo kati ya idara hiyo na wakunga kule mashinani.
Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2025 vifo 6 vya akina mama wakati wa kujifungua vilirekodiwa jimboni ikilinganishwa na vifo 5 vilivyorekodiwa mwaka 2024.
Hata hivyo Bokayo amesisitiza kuwa licha ya mafanikio hayo, juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha hakuna mama anayepoteza maisha kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.
Ametoa wito kwa akina mama kuhudhuria kliniki mapema na kujifungulia hospitalini ili kuzuia vifo hivyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya kaunti inayoongoza kwa vifo hivyo ni kaunti ya Garissa ikifuatwa na Mombasa, Isiolo, Lamu, na kisha kaunti ya Nyeri.
Kaunti zilizo na visa vichache zaidi ni kaunti ya Nyandarua ikufuatwa na Marsabit, Vihiga, Nandi, West Pokot na kisha kaunti ya Kimbu.
Aidha katika vifo vya watoto wachanga kaunti ya Marsabit ilirekodi visa 219 mwaka 2025 kati ya akina mama 8,990 waliojifungua. Hii ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo vifo 198 vya watoto wachanga vilirekodiwa kati ya akina mama 9,645 waliojifungua.
Bokayo amesema kuwa vifo hivi zimechangiwa na akina mama kukosa kuenda kliniki pamoja na kuchelewa kufika hospitalini wakati wa kujifungua.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanashirikiana na wahudumu afya wa nyanjani CHPs ili kuzuia maafa hayo.
Vifo vya uzazi husababishwa zaidi na kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua.



Post Comment