Mahakama ya leba mjini Nyeri imesitisha mgomo wa maafisa wa kliniki chini ya muungano wao wa KUCO, tawi la Marsabit kwa kipindi cha siku 30 zijazo.
NA SABALUA MOSES
Hatua hii inakusudia kutoa nafasi ya mazungumzo ya kina na ya nia njema kati ya maafisa hao wa kliniki na serikali ya kaunti ya Marsabit.
Uamuzi huo ulitolewa tarehe 10 mwezi huu wa Disemba katika kesi kati ya serikali ya kaunti ya Marsabit na maafisa wa kliniki tawi la Marsabit.
Muungano huo umesema kuwa umeheshimu na kukubaliana na uamuzi wa mahakama na kuonyesha utayari wa kushiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa malalamishi yao.
Mahakama pia imeagiza kuwa hakuna afisa wa kliniki anayepaswa kudhulumiwa, kuhamishwa, kutishwa, au kuchukuliwa hatua za nidhamu kwa kushiriki mgomo huo.
Vile vile vyama vyote viwili vinatarajiwa kujadili kwa uaminifu, kuwasilisha ripoti za maendeleo ndani ya siku 30.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 12 mwezi January 2026.



Post Comment