Loading Now

Highlights

KFS Marsabit yaonya wafugaji dhidi ya moto wa misituni msimu wa kiangazi

NA Nyabande Orwa

Msimu wa kiangazi ukiendelea katika kaunti ya Marsabit, idara ya huduma ya misitu nchini, KFS, tawi la Marsabit, imetoa tahadhari kwa wafugaji wanaolisha mifugo yao ndani ya misitu kuwa waangalifu ili kuzuia mikasa ya moto.

Kwa mujibu wa Kadiro Oche, afisa wa KFS anayesimamia utekelezaji wa sheria katika kaunti ya Marsabit, msimu wa kiangazi huongeza hatari ya moto wa misituni. Akizungumza na kituo hiki kwa niaba ya mkuu wa idara hiyo Marsabit, Kenneth Muthuri, Oche amesema baadhi ya visa vya moto husababishwa na wafugaji wanaovuna asali au wanaopambana na wadudu wa mifugo kama kupe, ambapo wakati mwingine hutumia moto.

Oche amesema idara hiyo imeimarisha doria na usalama katika misitu yote ya Marsabit kwa kushirikiana na wenzao wa KWS ili kuzuia uharibifu wa misitu. Maeneo yatakayopewa uangalizi zaidi ni Karare, Paskishon, Hulahula na Badasa.

Wakati huo huo, Oche amesema KFS tayari imefanya mikutano na machifu pamoja na jamii za wafugaji wanaoishi karibu na misitu katika maeneo ya Songa, Kituruni na Hulahula. Lengo ni kuhakikisha amani na matumizi salama ya misitu wakati wafugaji wanaporuhusiwa kuingia kusaka maji na malisho.

Post Comment