Homa ya influenza yazuka Loiyangalani na Sarima, wakazi waonywa kuchukua tahadhari
NA Nyabande Orwa
Wizara ya afya kaunti ya Marsabit imewataka wakazi wa Loiyangalani na Sarima, kaunti ndogo ya Laisamis, kuchukua tahadhari kutokana na mlipuko wa Influenza, homa kali inayosambaa haraka.
Akizungumza kwa simu na kituo hiki, Waziri wa Afya Malicha Boru amesema homa hiyo ilianza takriban wiki mbili zilizopita miongoni mwa wanafunzi wa shule na sasa imesambaa katika jamii.
Sampuli 23 zilipelekwa katika maabara ya KEMRI na kuthibitisha ugonjwa huo.
Boru amesema takribani watu 200 wameathirika kufikia sasa, lakini hakuna sababu ya taharuki. Serikali ya kaunti tayari imechukua hatua za kudhibiti maambukizi na maafisa wa afya wako mashinani kutoa huduma.
Waziri huyo amewataka wakazi kudumisha usafi, kunawa mikono mara kwa mara, na kufika hospitalini mapema wanapopata dalili kama kikohozi na mafua makali.
Wakazi wanashauriwa pia kuepuka mikusanyiko na kufuata ushauri wa kiafya ili kuepuka kuenea zaidi kwa ugonjwa.



Post Comment