Wazazi watafuta uhamisho kwa wanafunzi wa gredi ya 10 bila kuzingatia njia tatu za masomo, MarsabitÂ
NA Caroline Waforo
Wadau wa elimu katika kaunti ya Marsabit wameeleza wasiwasi mkubwa kuwa wazazi wengi hawazingatii njia tatu za masomo chini ya mtaala wa umahiri CBE, wanapotafutia wanao uhamisho hasa kwa wale walioteuliwa kujiunga na gredi ya 10 katika shule zilizo mbali.
Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti ya Marsabit Peter Magiri amesema kuwa wazazi wengi wanatafuta uhamisho huo, bila kuangazia uwezo na vipaji vya mwanafunzi, hali anayosema imechangiwa na ugumu wa maisha unaosababishwa na athari za kiangazi kinachoendelea kushuhudiwa katika kaunti ya Marsabit.
Magiri ameweka wazi kuwa, kwa sasa shule za Sekondari ya juu katika kaunti ya Marsabit zinatoa njia mbili pekee za masomo chini ya mtaala wa CBE, ambazo ni Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) pamoja na Sayansi za Kijamii
Hakuna shule inayotoa njia ya Sanaa na Michezo.
Kutokana na hali hiyo Magiri ametoa wito kwa viongozi kwa kaunti kushirikiana na idara ya Elimu ili kuwezesha shule za Sekondari ya Juu humu jimboni kutoa njia zote tatu za masomo.
Vilevile Magiri ametoa wito kwa wazazi na wadau mbalimbali wa elimu kutochanganya masuala ya elimu na siasa.
Haya yanajiri wakati ambapo tume ya kuwaajiri walimu TSC imefanya mageuzi ya uongozi katika shule mbalimbali jimboni Marsabit ikiwemo shule ya wavulana ya Marsabit.



Post Comment