Wakaazi wa Toricha Maikona walilia uhaba wa maji kutokana na visima kukauka. Waomba msaada kukabili janga hilo.
NA Samuel Kosgei
Wakazi wa maeneo ya Toricha na Qatamur katika Kaunti Ndogo ya Maikona, Kaunti ya Marsabit, wameiomba serikali pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kuingilia kati kwa dharura na kusaidia usafirishaji wa maji kwa malori, baada ya visima vya kukusanya maji ya mvua vya jamii pamoja na visima binafsi kukauka.
Wakazi wanasema hali hiyo imetokana na kufeli na kupungua kwa mvuakatika msimu wa mvua waOktoba, Novemba na Desemba.
Akizungumza na Radio Jangwani, kiongozi wa jamii ya Toricha Tumal Orto amesema zaidi ya familia 335 zimeathirika, huku watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu wakiathirika zaidi na uhaba huo wa maji.
Ameongeza kuwa barabara ya Maikona–Toricha iko katika hali mbaya sana, hali inayoongeza gharama ya kusafirisha maji, ambapo tanki la maji la lita elfu kumi linagharimu kati ya shilingi elfu kumi na saba hadi elfu ishirini.
Wakazi hao sasa wanatoa wito wa msaada wa haraka ili kupunguza athari za uhaba wa maji unaoendelea katika maeneo hayo.



Post Comment