Loading Now

Highlights

Wakaazi wa Songa waandamana kulalamikia ubovu wa barabara na huduma duni za afya.

NA JB Nateleng

Wakaazi wa eneo la Songa eneobunge la Saku kaunti ya Marsabit wamefanya maandamano leo Ijumaa kulalamikia ubovu wa barabara ya Badassa kuelekea Songa pamoja na huduma duni za afya katika eneo hilo.

Wakizungumza na Shajara wakaazi hao wamesema kuwa barabara hiyo imeharibika kwa muda mrefu, na imekuwa kero hasa kwa wakulima wanaosafirisha mazao yao kwenda sokoni.

Wamesema kuwa wanalazimika kutumia muda mwingi barabarani, na wakati mwingine mazao yao hufika yakiwa yameharibika hali inayowasababishia hasara kubwa.

Wakaazi hao wamewashutumu viongozi wa mashinani na wa jimbo kwa kuwapuuza na kushindwa kutafuta suluhu ya kudumu kwa barabara hiyo licha ya malalamishi ya muda mrefu.

Vilevile wamemtaka naibu rais Kithure Kindiki, kufuatilia ahadi aliyotoa alipokuwa Waziri wa Usalama kuhusu kuboreshwa kwa barabara hiyo.

Malalamisho hayo pia yametiliwa mkazo na chifu wa Songa, Abdi Dera, ambaye amesema kuwa ubovu wa barabara hiyo umechangia kuongezeka kwa visa vya uhalifu.

Amesisitiza kuwa ni jukumu la idara husika kuhakikisha barabara hiyo inakarabatiwa haraka ili kuimarisha usalama kwa wananchi.

Na kando na ubovu wa barabara wakaazi hao wamelalama ukosefu wa zahanati inayofanya kazi ipasavyo katika eneo hilo, ambapo sasa wamelazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya, jambo linalohatarisha maisha haswa kwa wagonjwa wa dharura.

Wameitaka serekali ya kaunti ya Marsabit kuangazia malalamishi yao kwa dharura.

Post Comment