Viongozi wa dini Marsabit wataka kampeni za amani kuelekea msimu wa siasa
Na Nyabande Orwa
Askofu wa kanisa la Kianglikana dayosisi ya Marsabit, Qampicha Wario Guyo, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa katika kaunti hii kuendesha kampeni za amani huku msimu wa siasa ukitarajiwa kuanza katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na kituo hiki kwa njia ya simu, askofu Qampicha amesema ni muhimu kwa wanasiasa kuwa waangalifu na matamshi yao ili kuepusha uchochezi unaoweza kusababisha uhasama wa kisiasa katika jamii.
Wito huo umeungwa mkono na Sheikh wa msikiti wa Jamia mjini Marsabit, Mohamed Noor, ambaye amewataka wanasiasa kuuza sera zao badala ya kuwagawanya wananchi kwa kutumia pesa.
Sheikh Noor pia amewahimiza raia kutokubali kutumiwa na viongozi wanaojinufaisha binafsi, na kuhudhuria mikutano ya kisiasa kwa amani kisha kurejea nyumbani.
Kwa upande wake, spika wa bunge la vijana katika eneo bunge la Saku, Abdiaziz Boru Tise, amewasuta vijana wanaokubali kutumiwa na wanasiasa. Amewaonya kuwa watawajibika wenyewe iwapo watajeruhiwa katika mikutano ya kisiasa.



Post Comment