Loading Now

Highlights

Ukosefu wa elimu kuhusu uhamiaji wachochea kuongezeka usafirishaji haramu wa binadamu

Na Caroline Waforo

Ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu uhamiaji umetajwa kuchochea ongezeko la usafirishaji haramu wa binadamu katika mpaka mwa Kenya na Ethiopia.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara kati ya jamii na maafisa wa polisi kuhusu usafirishaji wa binadamu ulioandaliwa katika uwanja wa Baraza Park leo Jumanne, Naibu Mkrugenzi wa idara ya uhamiaji katika eneo la Moyale Thomas Chalo amesema kuwa upande wa taifa jirani la Ethiopia umelegea katika kukabiliana na visa hivi.

Chalo amesema kuwa vita dhidi ya usafirishwaji wa binadamu vitafanikishwa kwa juhudi za pamoja kutoka mataifa yote mawili.

Kwa upande wake Lawrence Mugambi kutoka idara ya upelelezi DCI kitengo cha kukabiliana na ugaidi amewataka wazazi kuwajibika katika malezi ili kukomesha visa vya vijana kushawishika kujiunga na makundi haramu.

Katika mkutano huo, kina mama waliibua wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya wizi haswa nyakati za usiku na ambavyo vimezidi kushuhudiwa msimu huu wa mfungo wa Ramadhani.

Kutokana na malalamishi hayo, Naibu Kamishna wa Moyale Benedict Munywoki amewaamrisha mafichu kwa ushirikiano na maafisa wa akiba NPR kuimarisha doria nyakati za usiku ili kukomesha visa hivyo.

Aidha DCC Munywoki ametoa amri ya kufungwa kwa mabaa yote mjini humo baada ya saa tano usiku pamoja na huduma za bodaboda.

Mkutano huo umeandaliwa na shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa kupitia wizara ya usalama wa ndani.

Post Comment