Sindano ya Lenacapavir yaleta tumaini jipya katika mapambano dhidi ya HIV Marsabit
NA Nyabande Orwa.
Kuna manufaa makubwa katika matumizi ya sindano ya Lenacapavirinayosaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa watu walio katika hatari ya kuambukizwa.
Kwa mujibu wa mratibu wa idara ya kukabiliana na UKIMWI katika Kaunti ya Marsabit, Wario Galgalo, sindano hiyo ikianza kutumika kwenye kaunti hii itapunguza changamoto ya watu kumeza dawa kila siku, na itaongeza kinga kwa walio katika hatari ya maambukizi.
Akizungumza na kituo hiki katika kipindi cha Amkia Jangwani, Wario amesema kuwa kabla ya mtu kupewa sindano hiyo, lazima apimwe kwanza na kuchunguzwa na wahudumu wa afya ili kuhakikisha ni salama kwake.
Wakati huo huo, Wario amesema kuwa jumla ya watu 1,780 wameorodheshwa kuwa wanaishi na virusi vya HIV katika kaunti ya Marsabit hadi sasa.
Amesema kuwa unyanyapaa katika jamii ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya wagonjwa kuhamia kaunti nyingine kutafuta huduma.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya wanawake walioambukizwa iko juu kidogo kuliko ya wanaume kwa asilimia 0.7. Hata hivyo, amesema wanawake hujitokeza kwa wingi kupima na kutafuta huduma ikilinganishwa na wanaume.
Afisa huyo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima na kujua hali zao ili kusaidia kudhibiti maambukizi mapya.



Post Comment