Shirika la, MWADO, lazindua kitengo kipya cha nambari za dharura ili kukabili dhulma za kijinsia.
NA NYABANDE ORWA
Shirika la kutetea haki za binadamu, la Marsabit Women Advocacy & Develpoment Organisation, MWADO, limezindua kitengo kipya cha nambari za dharura kukabiliana na dhuluma za kijinsia katika eneo bunge la Saku, Marsabit. Kitengo hiki, kinachoitwa Directorate, kitasaidia waathiriwa kuripoti matukio kwa haraka na kupata msaada wa dharura.
Akiongea wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mkuu wa MWADO, Nuria Gollo, amesema nambari hizi zitasaidia kupambana na visa vya dhuluma za kijinsia katika eneo hilo.
Wakati huo huo, Afisa Mkuu wa Jinsia katika serikali kuu, Daki Dadacha, amesema kuwa serikali kuu ina mikakati ya kukabiliana na dhuluma za kijinsia na FGM kwa kushirikisha washikadau wote kwenye jamii, wakiwemo viongozi wa kidini, wazee wa jamii na vijana.
Hata hivyo, amesema mipaka isiyo rasmi imevuta nyuma juhudi hizo kwa sababu baadhi ya wakeketaji wanafanya tamaduni hiyo kisiri kwa kuvuka mpaka kuingia Ethiopia. Daki amepongeza hatua ya MWADO kuanzisha directorate hii, kwani itawasaidia wale wanaoogopa kuzungumzia visa vya dhuluma kutokana na unyanyapaa.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP, imesema kitengo hiki kitasaidia kuchunguza kesi zinazohusiana na dhuluma za kijinsia na kuwawajibisha wahusika kisheria. Edwin Otieno, mratibu wa ODPP Marsabit, ameeleza umuhimu wa kitengo katika kuharakisha ufuatiliaji wa kesi.
Kwa upande wa ofisi ya watoto kaunti ya Marsabit, hatua ya MWADO lakini pia kutoa wito wa kufuatilia utendaji wa kitengo hiki kila baada ya miezi sita ili kuhakikisha ufanisi kwa jamii.
Afisa huyo pia ametoa wito kwa serikali kuongeza idadi ya wafanyakazi kwenye idara hiyo ili kukabiliana kwa wakati na visa vya dhuluma, hasa miongoni mwa watoto.



Post Comment