Highlights

Serikali ya kaunti ya Marsabit yatenga shilingi milioni 260 kwenye bajeti ya ziada ili kupambana na athari za ukame

Na Caroline Waforo

Serikali ya kaunti ya Marsabit imetenga shilingi milioni 260 katika bajeti ya ziada ya mwaka 2025-2026 ili kupambana na athari za kiangazi zinazoendelea kushuhudiwa jimboni.

Fedha hizo zinatarajiwa kutumika katika usambazaji wa chakula cha msaada pamoja na maji kutumia malori kwa waathiriwa wa kiangazi.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge la Marsabit Daud Tomasot ambaye pia ni mwakilishi wadi wa Korr, bajeti hiyo ya shilingi bilioni 11 iliwasilishwa bungeni siku ya hapo jana Jumatano.

Katika makadirio hayo asimilia 60 ya bajeti ambayo ni shilingi bilioni 6.66 zimetengewa matumizi ya kawaida kama mishahara huku asilimia 40 ya bajeti ambayo ni shilingi bilioni 4.37 zikitengewa maendeleo.

Idara ya afya ndiyo imetengewa kiasi kikubwa cha fedha hii ikiwa ni shilingi bilioni 2.39 ambapo shilingi bilioni 2.19 zitatumika kwa matumizi ya kawaida huku milioni 202 zikitengewa miradi.

Idara nyingine ambayo imetengewa kiasi kikubwa cha fedha ni idara ya kilimo, ufugaji na uvuvi ambayo imetengewa shilingi bilioni 1.5 huku idara ya fedha ikitengewa bilioni 1.2

Kamati hiyo ya bajeti inatarajiwa kuandaa kikao cha ushirikishwaji wa umma kesho Ijumaa kabla ya bajeti hiyo ya ziada kuidhinishwa na kutekelezwa.

Post Comment