Highlights

Msimu wa Kwaresma na Ramadhan waanza hii leo wakristu wakiadhimisha jumatano ya majivu.

Na JB Nateleng

Msimu wa Kwaresma umeanza rasmi leo, Jumatano ya Majivu, huku waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Marsabit wakihimizwa kujitoa katika sala, kufunga na kufanya matendo ya toba kwa kipindi cha siku 40 zijazo.

Akizungumza katika Parokia ya Loglogo, Jimbo Katoliki la Marsabit, Baba Paroko Padri Steve Mutuku amesema Kanisa linawaalika waumini kudumu katika sala na kuliombea taifa, hasa katika kipindi hiki ambacho joto la kisiasa linaanza kushika kasi nchini.

Padri Mutuku amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila muumini kutumia siku hizi 40 zilizotengwa na Kanisa kujiombea binafsi na kuwaombea wengine wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali, ili Mwenyezi Mungu awape ulinzi na kuwatimizia mahitaji yao.

Aidha, Padri Mutuku amezitaka familia kutumia kipindi hiki kuimarisha mshikamano wa kifamilia kwa kuwa karibu na watoto wao pamoja na wanajamii. Amekosoa matumizi ya muda mwingi katika mitandao ya kijamii, akisema hali hiyo inachangia kudorora kwa maadili mema katika jamii.

Vilevile, amewahimiza waumini kujitolea katika matendo ya huruma kwa kuwasaidia wasiojiweza, kuwatembelea wagonjwa, wafungwa gerezani na mayatima kama sehemu ya kuishi kiimani.

Kwaresma ni kipindi maalum katika kalenda ya Kanisa kinachoanza baada ya Jumatano ya majivu kwa lengo la kuwaandaa Wakristu kufuata nyayo za mwokozi Yesu Kristo kupitia njia ya msalaba pamoja na mafundisho matakatifu yanayolenga kukuza na kuimarisha imani.

Kwaresima itahitimishwa katika kipindi cha Pasaka kitakachoanza tarehe 5 Aprili 2026.

Post Comment