Huduma za vitambulisho kuanza Korr Wiki Ijayo.
Na Nyabande Orwa
Afisa mkuu anayesimamia huduma za usajili wa vitambulisho katika kaunti ya Marsabit, Isaac Kibet, amesema idara yake iko mbioni kuhakikisha kuwa wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18 wanapata kitambulisho cha kitaifa.
Kibet amesema ofisi yake imeweka mikakati ya kuanza kutoa huduma hizo katika kaunti ndogo ya Korr kuanzia wiki ijayo. Tamko lake linajiri baada ya wakazi wa eneo hilo kulalamikia ukosefu wa huduma za usajili tangu kuanzishwa kwa kaunti hiyo ndogo hivi karibuni.
Akizungumza na meza yetu ya habari, Kibet amesema walilazimika kutafuta maafisa zaidi wa usajili ili kukidhi mahitaji ya wakazi, na sasa maandalizi hayo yamekamilika.
Wakati huo huo, amesema wanashirikiana na tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC, kuwasajili wananchi kama wapiga kura mara tu wanapopata vitambulisho vya kitaifa.
Aidha, Kibet amesema baada ya kuondolewa kwa mchakato wa kupigwa msasa, imekuwa rahisi kwa wananchi kupata kitambulisho. Amesema wanaohitaji kitambulisho wanapaswa kuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa chifu pamoja na nakala ya kitambulisho cha mzazi mmoja.
Kwa wazee wanaotumia vitambulisho vya zamani, wametakiwa kuvirejesha ofisini ili wapewe vya kisasa.



Post Comment