Gavana Mohammud Ali itaka idara ya usalama kuwakamata waliotekeleza mauaji katika migodi ya Hillo
Na Sabalua Moses
Gavana wa kaunti ya Marsabit Mohamoud Ali ameitaka idara ya usalama kuimarisha usalama kote jimboni na kuhakikisha kuwa waliotekeleza mauaji ya hivi maajuzi katika migodi ya Hillo iliyoko katika eneobunge la Moyale, wamekamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa chakula cha msaada kwa waathiriwa wa ukame leo Jumatatu, Gavana Ali ameituhumu idara ya usalama kwa kile anadai ni kuhangaisha raia wasiokuwa na hatia.
Katika uzinduzi huo Gavana Ali pia amekashifu tukio la majuma kadhaa yaliyopita ambapo wakaazi wa Bori waliandamana kulalamikia ukosefu wa maji na huduma duni za afya akisema kuwa tukio hilo lilichochewa kisiasa kwani serikali ya kaunti ilikuwa ikisambaza maji kutumia malori kwa wakaazi hao.
Na kutokana na makali ya kiangazi yanayoendelea kushuhudiwa jimboni na hata katika maeneo mengine nchini, naibu gavana wa Marsabit Solomon Gubo ameitaka serikali kuu kutangaza ukame kuwa janga la kitaifa
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau ambaye amesema kuwa serikali ya kuu itashirikiana na ile ya kaunti ya Marsabit pamoja na wahisani wengine katika usambazaji chakula cha msaada na maji.
Vilevile amewataka wahisani zaidi kujitokeza na kusaidia katika ukarabati wa visima vilivyoharibika jimboni.
Kadhalika ametoa wito wa amani msimu huu wa ukame ambapo mizozo ya malisho huongezeka kutokana na uhaba wa maji na lishe.
Leo hii serikali ya kaunti ya Marsabit imesambaza msaada wa magunia 6,300 ya mchele na magunia 3,100 ya maharagwe kwa waathiriwa wa ukame katika wadi zote 20 jimboni.



Post Comment